Wednesday, 7 September 2016

VIUNGO VYA MTOTO MCHANGA VYAZAGAA MTAANI SHINYANGA


 
VIUNGO vinavyodhaniwa kuwa ni vya mtoto mchanga vimeonekana kuzagaa katika mtaa wa Butengwa, Kata ya Ndembezi, Manispaa ya Shinyanga bila kufahamika ni nani aliyesababisha vizagae.Mwenyekiti wa mtaa huo, Juma Derefa alisema kuwa jana saa 5:00 asubuhi waliona viungo vya mtoto mchanga vikiwa vimezagaa mtaani na kutoa taarifa.
 
Derefa alisema baadhi ya viungo vilikuwa vimebebwa na mbwa na baada ya kuona hivyo, walifuatilia.“Viungo hivyo vimeonekana mbali na makazi ya watu jirani wa kwenye mtaa wa Mwadui. Viongozi wake tumewashirikisha na hadi sasa hatujamtambua aliyefanya kitendo hicho cha kikatili cha kutupa au kutelekeza viungo hivyo,” alisema.

Alisema huenda wananchi wanafahamu nani aliyekuwa na mtoto au mjamzito na kufanya kitendo hicho.

“Ndio tumeanza uchunguzi kwa kushirikiana na Polisi,” alisema Derefa.

Diwani wa kata hiyo David Nkulila alisema tukio hilo alilipata baada ya kupewa taarifa na mmoja wa mjumbe wa serikali ya mtaa huo kuwa viungo vya mtoto mchanga vimebainika kuzagaa hovyo mitaani huku vingine vikiwa vimeng’atwa na mbwa lakini alishirikiana na viongozi wengine wa kata na kutoa taarifa jeshi la polisi.

“Sasa sisi tumeanza uchunguzi kwa kushirikiana na jeshi la polisi na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano wa kubaini kichanga hicho kilitupwa na mhusika ni nani je? kilitupwa kikiwa hai au kimekufa hicho nacho tunafuatilia”,alisema Nkulila.

Kaimu kamanda wa jeshi la polisi mkoani hapa Elias Mwita alisema kuwa taarifa hizo wamezipata na wameanza kuzifanyia uchunguzi.
Post a Comment

Our Team

Video of the Day

Contact us

Name

Email *

Message *