Tuesday, 13 September 2016

Mabweni mawili ya Shule ya Sekondari Ambassador Iliyopo Tabata Segerea, Yameteketea kwa Moto


 Image result for Shule ya Sekondari Ambassador Tabata Segera
Mabweni mawili ya Shule ya Sekondari Ambassador iliyopo Tabata Segerea, yameteketea kwa moto juzi saa tatu usiku na kusababisha hasara ya takriban Sh1.5 bilioni.
Mkurugenzi wa shule hiyo, Omary Mkwarulo alisema makadirio ya hasara hiyo yanatokana na thamani ya jengo na mali zilizokuwamo ambazo ni vitanda 400, mashuka 1,200, taulo, mito pamoja na mali nyingine za wanafunzi.
“Shule yangu ina wanafunzi 240 lakini wote walikuwa wamefunga shule tangu tarehe 10, mwezi huu na kwa kuwa ilikuwa ni likizo fupi wengi waliacha mali zao ambazo nazo zimeteketea kwa moto,” alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni alisema mpaka sasa uchunguzi wa chanzo cha moto huo bado unaendelea.
Licha ya kwamba chanzo cha moto huo bado hakijafahamika, Mkwarulo alilihusisha tukio hilo na wivu wa kibiashara kwa madai kwamba huenda wapinzani wake ndio wamechoma majengo hayo. “Nahisi ni wivu wa kibiashara kwani hivi karibuni nilipata wanafunzi wa kigeni wenye asili ya Australia... sasa labda watu wanaona wivu shule yangu kuendelea kuaminiwa,” alisema Nkwarulo.
Hata hivyo, alisema timu ya wataalamu itafanya kazi ya tathmini leo kujua hasara iliyopatikana na baada ya hapo ujenzi au ukarabati wa majengo hayo utaanza mara moja ili shule itakapofunguliwa Septemba 19 wanafunzi wakute mazingira yao ya kulala yameshatengenezwa.
Mmoja wa wazazi wa wanafunzi wa shule hiyo, Jumanne Ahmad alisema ajali hiyo itamgharimu kiuchumi kwani atalazimika kununua baadhi ya mahitaji ya mtoto wake ambayo alikuwa ameshayatimiza.
“Uzuri ajali imetokea watoto wakiwa likizo, hivyo hakuna madhara kiafya, lakini kwa upande wa mwanangu nimepata hasara ya kifedha kwani nitalazimika kutafuta ada na pesa ya mahitaji mengine kwani karibia vitabu vyote na baadhi ya nguo vimeteketea,” alisema Ahmad.
Tukio hilo limetokea siku chache baada ya bweni la wasichana la Shule ya Sekondari Mwanzi wilayani Manyoni Mkoa wa Singida, kuteketea kwa moto na kusababisha hasara ya zaidi ya Sh50 milioni huku wanafunzi 42 wakinusurika. Bweni hilo la shule pekee wilayani humo yenye kidato cha tano na sita, liliteketea juzi saa 2.20 usiku.
Post a Comment

Our Team

Video of the Day

Contact us

Name

Email *

Message *