Tuesday, 9 August 2016

MPYA: Majina ya wanafunzi wasio na sifa vyuo vikuu hadharani

SERIKALI imesema majina ya wanafunzi waliojiunga na vyuo vikuu bila kuwa na sifa yatatangazwa mwezi ujao na kuondolewa masomoni, baada ya uhakiki wake kukaribia kukamilika.
Katika mahojiano maalum na Nipashe jana, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako alisema ameshawaagiza watendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) kufanyia kazi suala hilo.
Ili kuwabaini wanafunzi wote wasio na sifa, waziri huyo alisema tayari tume hiyo imeanza uhakiki vyeti vya wanafunzi wote waliopo vyuoni.
Profesa Ndalichako alisema uhakiki huo unafanywa kwa kuangalia vyeti vya wanafunzi walioingia katika vyuo hivyo pamoja na kuhakiki kwa njia ya mtandao.
"TCU ndiyo wanafanya kazi hiyo na wana 'data' (takwimu) zaidi, unaweza kuwauliza, lakini ninachofahamu kuna hatua ambazo wameanza kuzifanya, kuangalia vyeti na pia kupitia usajili wao kwa njia ya mtandao," alisema Prof. Ndalichako.
Kuhusu uhakiki wa wanafunzi hewa, kiongozi huyo wa serikali alisema "mchakato huo bado unaendelea".
Ingawa hakutaka kulizungumzia kwa undani suala hilo kwa maelezo kuwa si msemaji wa TCU, Kaimu Mkurugenzi wa Udahili na Nyaraka wa tume hiyo, Dk. Kokubelwa Mollel, alisema majina ya 'vihiyo' waliopo vyuo vikuu yataanza kuanikwa mwezi ujao baada ya kumalizika kwa udahili wa wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa masomo wa 2016-17 unaofanyika sasa.
"Tulitakiwa tuanze mapema mwezi huu kuwafichua wanafunzi walio kwenye vyuo bila sifa zinazotakiwa, lakini likaja suala la kudali wanafunzi kwanza na ndiyo kazi ambayo tunaifanya sasa," alisema.
"Tukimaliza kazi hii Agosti 31, tutaanza kazi hiyo ya kuhakiki wanafunzi walioingia vyuoni bila sifa," alisema.
Uhakiki wa wanafunzi walipo vyuoni nchini, unafanyika ikiwa ni wiki chache tangu Prof. Ndalichako atangaze serikali imebaini kuwapo kwa wanafunzi 'hewa' na 'vihiyo' ambao wanapatiwa mikopo na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).
Prof. Ndalichako pia alifuta udahili wa wanafunzi 7,423 waliokuwa wamedahiliwa kusoma stashahada ya ualimu wa sayansi katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) pasi na sifa.
Akitangaza uamuzi huo wa kuwaondoa Udom wanafunzi hao katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Dodoma Mei 25, Prof. Ndalichako alisema serikali itafanya msako kwenye vyuo vyote nchini kuwabaini wanafunzi wasio na sifa za kusoma elimu ya juu.
Prof. Ndalichako alisema msako huo hautaishia kwa wanafunzi waliopo vyuoni, bali utawagusa hata wahitimu walioko kazini ikiwa walipata vyeti vyao baada ya kujiunga na elimu ya juu kwa njia za udanganyifu.
"Sifa zote za wanafunzi walioko vyuo vikuu ninazo kwenye kompyuta yangu," Prof. Ndalichako alisema "Kama kuna watu wanafahamu waliingia vyuoni kwa ujanja ujanja, ni bora wasipoteze muda wao na rasilimali zao kuendelea kujigharimia wakati wanajua wameingia na sifa zisizo sahihi maana tunaenda kuwanyofoa."
Post a Comment

Our Team

Video of the Day

Contact us

Name

Email *

Message *