TAARIFA KWA UMMA KUTOKA IKULU,ISOME TAFADHALI | MASWAYETU BLOG
Breaking News
Loading...
Millionaire  Ads

Friday, 3 June 2016

TAARIFA KWA UMMA KUTOKA IKULU,ISOME TAFADHALI

INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU

Simu : +255-22-2114512, 2116898
Email : press@ikulu.go.tz
Tovuti : www.ikulu.go.tz
Faksi : 255-22-2113425
OFISI YA RAIS,
IKULU,
1 BARABARA YA BARACK OBAMA,
11400 DAR ES SALAAM,
TANZANIA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema serikali yake ya awamu ya tano itahakikisha wanafunzi wa vyuo vikuu wanapatiwa mikopo, lakini haitakubali kulekeza mikopo hiyo kwa wanafunzi wasiokuwa na sifa za kujiunga na vyuo vikuu.
Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo tarehe 02 Juni, 2016 wakati akizungumza na Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam muda mfupi baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa maktaba ya kisasa ya chuo hicho inayojengwa katika kampasi ya Mlimani upande wa mashariki mwa chuo.
Akiwahutubia maelfu ya wanajumuiya hiyo wanaojumuisha wanafunzi, wahadhiri na wafanyakazi wa chuo, Dkt. Magufuli amesema serikali yake imedharia kutoa elimu bora kwa watanzania na imejipanga kuhakikisha inakabiliana na changamoto mbalimbali zinazovikabili vyuo, lakini ameelezea kusikitishwa kwake na uwepo wa wanafunzi waliodahiliwa na baadhi ya vyuo hapa nchini pasipo kuwa na sifa zinazomwezesha mwanafunzi kujiunga na chuo kikuu.
"Wapo wanaokopeshwa mikopo hii ya elimu ya juu lakini hawana sifa, Mheshimiwa Profesa Ndalichako (Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi) nakushukuru kwa hatua unazozichukua katika kusafisha wizara yako na hili nalisema kwa uwazi, na ukweli lazima usemwe hata kama ni mbele ya wanachuo.
"Una D,D unasajiliwa kuchukua digrii chuo kikuu na unapata mkopo wa serikali, ni aibu ya ajabu, haiwezekani, haiwezekani, haiwezekani. Lakini wakati tunawalipia wanafunzi 489 waliomaliza kidato cha nne na kupata D,D manaake wengine ni divisheni 4, kuchukua digrii, wapo wanafunzi wengine wa kidato cha sita wamekosa mikopo, wapo wanafunzi wengine walio na diploma wamekosa mikopo" Amesema Rais Magufuli.
Rais Dkt. John Pombe Magufuli pia amewataka wanafunzi wa vyuo mbalimbali hapa nchini kuacha kujihusisha na masuala ya siasa na badala yake wazingatie jukumu kuu lililowapeleka vyuoni ambalo ni kusoma, huku akibainisha kuwa serikali yake haitavumilia vitendo vya vurugu vyuoni.
"Ifike mahali watanzania tukubali ukweli, tuache siasa kwenye masuala ya msingi, ukimpeleka mwanafunzi wa kidato cha nne mwenye ufaulu wa divisheni 4, anachukua digrii, akishatoka pale, hata kama atafanikiwa kupata digrii itakuwa ni ajabu.
"Lakini niwaombe wanafunzi mahali kote, msitumiwe na wanasiasa, mmekuja kusoma, someni, siasa mtazikuta mkiondoka, nawambia mmekuja kusoma someni, na ndio maana hata katika kutoa mikopo hatubagui, sijui huyu CCM, sijui huyu CHADEMA, sijui huyu nini, nyie wote ni watanzania, ndio lengo letu. Amesisitiza Dkt. Magufuli.
Amewaahidi kuwa serikali yake itahakikisha inatoa mahitaji ya wanafunzi ikiwemo mikopo na kuboresha miundombinu ya vyuo, lakini amewataka wanavyuo nao kuwa wavumilivu na wazalendo pale ambapo mahitaji hayo yatachelewa kutokana na mchakato wa kuyapata kuhitaji muda.
Kabla ya kuwahutubia wanajumuiya ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Mkuu wa chuo hicho ambaye ni Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemuomba Rais Magufuli asaidie kuboresha miundombinu ya chuo hicho ikiwemo ujenzi wa mabweni ya wanafunzi ambao kwa takribani asilimia 70 wanaishi nje ya chuo, ambapo Rais Magufuli ameahidi kutoa shilingi bilioni 10 na ameuagiza uongozi wa chuo hicho kuainisha eneo ndani ya chuo ili ujenzi wa mabweni uanze mara moja.
Uzinduzi wa ujenzi wa Maktaba hiyo ya kisasa umehudhuriwa na Balozi wa China hapa nchini Dkt. Lu Youqing ambaye nchi yake ndio imetoa msaada wa dola za Marekani zaidi ya Milioni 41 kwa ajili ya ujenzi wa Maktaba hiyo.
Maktaba hiyo ya kisasa itakapokamilika itakuwa ndio maktaba bora kuliko zote barani Afrika, ikiwa na ukubwa wa eneo la meta za mraba 20,000 na itakuwa na uwezo wa kuwa na vitabu 800,000 na kuchukua wanafunzi 2,600 kwa mpigo.


Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
BONYEZA HAPA KUDOWNLOAD APPLICATION MPYA YA MASWAYETU BLOG

google+

linkedin

About Author
  • Donec sed odio dui. Duis mollis, est non commodo luctus, nisi erat porttitor ligula, eget lacinia odio sem nec elit. Sed posuere consecteturDonec sed odio dui. Duis mollis, est non commodo luctus, nisi erat porttitor ligula, eget lacinia odio sem nec elit. Read More

    0 comments:

     

    About Us