Thursday, 12 May 2016

WATU 7 WAUAWA SENGEREMA KWA KUKATWA MAPANGA

INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
Watu saba wa familia moja katika kitongoji cha Nyigumba kijiji cha Sima wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, wameuawa kwa kukatwa katwa mapanga usiku wa kuamkia leo.
Tukio hilo lililoacha simanzi katika kitongoji hicho, limehusisha ndugu watano wa tumbo moja wakiwamo wanafunzi watatu, waliovamiwa usiku wa manane na watu wasiojulikana na kuanza kucharangwa mapanga.
 
Baadhi ya wakazi wa kitongoji hicho wamesikitishwa na tukio hilo ambalo limetokea majira ya saa tisa usiku wa kuamkia Mei 11, huku wakiiomba serikali kuchukua hatua kali dhidi ya watu watakaobainika kuhusika na mauaji hayo.
 
Inadaiwa kuwa watu wawili waliokuwa na mapanga walikwenda katika nyumba ya wanafamilia hao na kuanza kuwashambulia huku wakianza na marehemu Donald ambaye alipambana na wauaji hao lakini alizidiwa nguvu kabla ya kuangushwa chini na kukatwa katwa mapanga, huku mama wa familia hiyo ambaye naye ameuawa katika tukio hilo akijaribu kufungua mlango wa chumba walicholala wajukuu na watoto wake, hali iliyowapa mwanya wauaji hao kuingia ndani ya nyumba hiyo na kuanza kuwashambulia kwa mapanga.
 
Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama amefika katika eneo la tukio na kusema kitendo kilichofanywa na wauaji hao hakiwezi kuvumiliwa.
 
Kwa mujibu wa diwani wa kata ya Sima Makoye Lugata watu waliouwa ni pamoja na mama mwenye nyumba Augenia Kiwitega, Maria Philipo na Leonard Thomas ambaye anasoma kidato cha nne katika shule ya sekondari Sima, wengine ni Leornad Aloys mwanafunzi wa darasa la saba, Mkiwa Philipo wa darasa la tano katika shule ya msingi Ijinga.
 
Marehemu wengine wamefahamika kwa jina moja la Samson na Donald kutoka wilayani Ngara mkoani Kagera ambao walikuwa wanafanya kazi ya kilimo kwenye familia hiyo.
 
Katika tukio hilo watoto wawili (majina yamehifadhiwa) wa familia hiyo wamenusurika kuuawa baada ya kujificha chini ya uvungu wa kitanda.
Post a Comment

Our Team

Video of the Day

Contact us

Name

Email *

Message *