Saturday, 12 March 2016

Uchaguzi wa Meya Jiji la Dar kufanyika Kabla ya Tarehe 25 Mwezi Huu

INNOCENT-THE BLOGGER-BOYHatimaye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene amemaliza mzozo wa uchaguzi wa meya wa Jiji la Dar es Salaam baada ya kuagiza ufanyike kabla ya Machi 25 na kutaja sifa za wapigakura.


Uamuzi huo wa kutangaza tarehe na sifa za wapigakura unaonekana kuwa ahueni kwa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ambavyo vilifurahia hatua kama hiyo, lakini wadau wa CCM wakafungua kesi iliyosababisha uchaguzi huo uahirishwe mara tatu.


Simbachawene, ambaye aliwahi kuagiza uchaguzi huo ufanyike kabla ya Februari 29 lakini ukakwama mara tatu, aliwaambia waandishi wa habari jana mjini Arisha kuwa uchaguzi huo utafanyika kwa kuzingatia kifungu cha 13 (1) cha Kanuni za Kudumu za Jiji.


Alisema watakaopiga kura katika uchaguzi huo ni madiwani wote wa halmashauri za jiji la Dar es Salaam ambazo ni Ilala, Temeke na Kinondoni, wabunge wa kuchaguliwa na wabunge wa viti maalumu ambao mchakato wa kuwapata ulianzia kwenye mamlaka za halmashauri hizo.


Simbachawene alisema wapigakura wengine watakuwa ni wabunge wa kuteuliwa na Rais, ambao ni Dk Philip Mpango, Balozi Agustine Mahiga, Dk Ackson Tulia, Profesa Joyce Ndalichako, Dk Abdallah Possi, Profesa Makame Mbarawa ambao ni wakazi wa jijini Dar es Salaam.


“Tunaomba vyama kuheshimu misingi ya demokrasia kwa kukubali matokeo ili kutosimamisha maendeleo ya jiji la Dar es Salaam,” alisema.


Taarifa ya tarehe ya uchaguzi huo na sifa za wapigakura imepokewa vizuri na viongozi wa Ukawa, ambao walitaka tamko hilo litolewe ndani ya siku saba na Serikali ibainishe sifa za wajumbe watakaoingia kupiga kura.


Kwa uamuzi huo wa Simbachawene, Ukawa, ambayo ina madiwani na wabunge kutoka vyama vya CUF na Chadema, itaingia kwenye uchaguzi ikiwa na wapigakura 87, huku CCM ikiwa na 76.


Akizungumza baada ya kupata taarifa hizo jana, Katibu wa Chadema Mkoa wa Dar es Salaam, Henry Kilewo alisema Simbachawene amesikia agizo lao walilotaka kupewa mapema tarehe ya uchaguzi huo.


“Kimsingi zile siku saba zilikuwa zinaisha leo (jana). Kwa hiyo Waziri Simbachawene ametumia busara. Hivyo ndivyo kiongozi anatakiwa kuwa,” alisema Kilewo.


Kilewo aliitaka CCM kujianda kisaikolojia, akisema wasitarajie ushindi kwa kuwa licha ya kuongezewa wajumbe, Ukawa bado wana hazina kubwa ya wajumbe.


“Tumeshapata taarifa kuwa wamepanga kuwakamata baadhi ya wajumbe wetu ili idadi ipungue. Nawaambia wasisithubutu kufanya mchezo huu bali wakubali yaishe na kuachia jiji,” alisema Kilewo.


Kwa takriban miezi miwili, uchaguzi katika jiji la Dar es Salaam umesimama kutokana na mvutano baina ya CCM na Ukawa, hasa wa uhalali wa wajumbe halali wa kupiga kura.


Kutokana na mgogoro huo, wabunge watatu wa Chadema, Halima Mdee wa Kawe, Mwita Waitara (Ukonga) na Said Kubenea (Ubungo) wameshtakiwa kwa tuhuma za kusababisha vurugu baada ya kusitishwa uchaguzi huo hivi karibuni kwa kutumia zuio hilo ambalo limebainika kuwa batili.


Akizungumzia zuio hilo, Simbachawene alisema lilikuwa ni batili kwa kuwa lilitolewa wakati tayari kesi ya msingi ilikuwa imetolewa uamuzi tangu Februari 23.
Post a Comment

Our Team

Video of the Day

Contact us

Name

Email *

Message *