Saturday, 26 March 2016

Kificho Ang’oka Uspika

INNOCENT-THE BLOGGER-BOY


Pandu Ameir Kificho
ALIYEKUWA Spika wa Baraza la Wawakilishi kwa zaidi ya miaka 20 sasa, Pandu Ameir Kificho, ameng’olewa katika nafasi hiyo baada ya kushindwa katika kura za kuwania awamu nyingine ya uongozi wa baraza hilo.

Badala yake wajumbe wateule wa Baraza la Wawakilishi, wamemchagua Zubeir Ali Maulid, kuwa Spika mteule wa baraza hilo, baada ya kupata kura 55 na kumuacha kwa mbali Kificho aliyeambulia kura 11 katika uchaguzi uliofanyika jana katika Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui, Zanzibar.

Aidha katika uchaguzi huo ambao wawakilishi 72 walipiga kura, Janeth Nora Sekihola ambaye ni hakimu mstaafu akipata kura 4 wakati kura mbili ziliharibika.

Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuangushwa katika uchaguzi huo, Kificho alisema amekubali kushindwa na yupo tayari kutoa ushirikiano akitakiwa kufanya hivyo.

“Hiyo ndiyo demokrasia, nimekubali kushindwa na nipo tayari kutoa ushirikiano mkubwa nikitakiwa kufanya hivyo kwa sababu ni ukweli kwamba ninao uzoefu mkubwa katika nafasi hiyo kwa zaidi ya miaka 20,” alisema.

Naye Spika mteule wa baraza hilo, Maulid alisema anakabiliwa na changamoto kubwa ya kuleta maendeleo na mabadiliko makubwa katika chombo hicho ambacho ni moja ya mihimili ya dola katika utekelezaji wa majukumu yake.

Amesema atatumia uzoefu alioupata kufanya kazi katika taasisi za kutunga sheria, kwa ajili ya kuleta mabadiliko hayo kwa kuhakikisha kwamba Baraza la Wawakilishi linafanya kazi inayotakiwa ya kuisimamia Serikali kwa mujibu wa Katiba.

“Nimekuwa Mwakilishi Shauri Moyo na Waziri mwaka 2000, pia nimekuwa Mwenyekiti wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa miaka miwili na nusu kwa hivyo uwezo wa kufanya kazi katika mabunge ya Jumuiya ya Madola ninao mkubwa,” alisema.

Aliwaomba wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wateule kumpa kila aina ya ushirikiano utakaomwezesha kutekeleza na kutimiza majukumu yake kwa mujibu wa Katiba, kwani chombo hicho ni moja ya mihimili ya dola.

Baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliozungumza na gazeti hili, wamesema kwamba mabadiliko hayo ni ishara na ujumbe tosha kwa Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kwamba wawakilishi wanataka mabadiliko makubwa kwa Serikali kwa ajili ya kuwatumikia wananchi.

“Mabadiliko makubwa tuliyoyafanya sisi wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa kumchagua Zubeir Ali Maulidi kuwa Spika mteule mpya, ni dalili tosha kwamba sasa tunataka mabadiliko makubwa ndani ya Serikali kwa kuwa na viongozi watakaowatumikia wananchi moja kwa moja,” alisema Rashid Ali Juma mwakilishi mteule wa jimbo la Amani.

Kificho ameweka historia kuwa Spika wa Kwanza katika Baraza la Wawakilishi la mfumo wa vyama vingi kuanzia mwaka 1995, ambapo kabla ya kuchaguliwa kushika wadhifa huo, alikuwa mwakilishi wa Jimbo la Makunduchi kuanzia 1988.

Zubeir Ali Maulid mwaka 2000 alichaguliwa kuwa Mwakilishi wa Shauri Moyo kwa tiketi ya CCM na kuteuliwa kuwa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, chini ya Serikali ya Rais mstaafu Amani Abeid Karume, ambapo alidumu katika wadhifa huo kwa miaka mitatu.

Mwaka 2005, Zubeir alichaguliwa kuwa Mbunge wa Kwamtipura kwa tiketi ya CCM ambapo akiwa bungeni katika kipindi cha miaka miwili na nusu, alikuwa Mwenyekiti wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na kuongoza vikao mbali mbali kwa kusaidiana na spika na naibu spika.

Katika hatua nyingine, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein, amemteua Said Hassan Said, kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ). Uteuzi huo ndio wa kwanza kufanyika, tangu Rais Shein alipokula kiapo cha kuongoza Zanzibar kwa miaka mitano ijayo Alhamisi ya wiki hii.
Post a Comment

Our Team

Video of the Day

Contact us

Name

Email *

Message *