Monday, 1 February 2016

Waziri Alipokiri Kuwa Mchawi-39

INNOCENT-THE BLOGGER-BOY

ILIPOISHIA IJUMAA:
“Basi wewe nenda.”
Mlinzi akatoka. Mimi niliogopa kurudi chumbani, nikaenda kukaa sebuleni. Niliogopa kurudi chumbani kwa sababu nilijua mke wangu alikuwa akinisubiri anishambulie kwa maneno na ugomvi wake ungekuwa mkubwa.
Pale sebuleni nilifungua TV, nikawa ninatizama taarifa mbalimbali za nje. Usingizi ulikuwa umeniruka.SASA ENDELEA…
Wakati nimekaa hapo nilisikia sauti ya mke wangu akizungumza kwenye simu chumbani. Sikuweza kujua alikuwa akizungumza na nani.
Alizungumza kwa muda mrefu kisha akatoka akiwa amembeba mwanaye. Kilichonishangaza ni kuwa alikuwa amevaa nguo zake za kutokea kama vile alikuwa anataka kwenda mahali.
Nikatazama saa iliyokuwa ukutani. Ilikuwa ikikaribia kuwa saa kumi na moja na nusu.
Kwa jinsi uso wake ulivyokuwa ameukunja sikuweza kumuuliza kitu.
Aliketi kwenye kochi kisha akaniambia.
“Baba Mkanga mimi naondoka kwenye nyumba hii.”
“Unataka kwenda wapi saa hizi?” nikamuuliza huku macho yangu yakiwa kwenye skriini ya TV.
“Ninakwenda kwetu. Siwezi kuendelea kuishi na wewe. Nakuacha uendelee na mambo yako.”
“Niendelee na mambo yangu yapi mke wangu?”
“Haya matatizo yote yanayotokea hapa nyumbani tangu juzi umeyasababisha wewe…” mke wangu alikuwa akiendelea kusema, nikamkatiza.
“Nimeyasababisha mimi kivipi?”
“Usinifanye mimi ni mjinga mume wangu. Mimi nimeshajua kuwa wale watu wanaokuja ni wenzako kama walivyosema wenyewe, wanatoka kwenu Nzega!”
“Wakitoka kwetu Nzega ndiyo wenzangu. Inawezekana wametumwa tu na maadui zangu waje waniharibie kazi.”
“Jana kuna mmoja alisema wazi kuwa mlikuwa mnafukua makaburi pamoja. Kufukua makaburi maana yake nini?”
“Wewe mwenyewe unaona kuwa hayo maneno hayaeleweki. Mimi waziri mzima nifukue makaburi?” nikajidai kumuuliza.
“Wale ni wachawi na wewe ni mwenzao kama walivyosema wenyewe. Mlikuwa mnafukua makaburi pamoja usiku ukienda huko kwenu.”
Mke wangu aliponiambia hivyo niliona aibu nikaugeuza uso wangu kuelekea kwenye sikriini ya TV.
“Umeahidi kumtoa mtoto wako kama kafara kwa wachawi wenzako, sasa leo unajidai kuwageuka wenzako!” Mke wangu aliendelea kuniambia kwa hasira. Machozi yakaanza tena kumtoka.
“Hayo ni maneno yako wewe, mimi si mchawi. Wale watu wametumwa kuja kunichafua tu kwa sababu zao.”
“Mume wangu wewe ni mchawi, usikatae!” Mke wangu akaniambia kwa mkazo na kwa sauti ya juu.
“Nitakataa, nisikatae kwa nini makatio mimi si mchawi.”
“Kabla ya hawa wachawi kuja hapa nilikwisha kutilia shaka. Kumbuka kuna siku niliamka usiku nikawa nakutafuta nikakukuta uko uchi uani umeufungua ule mkoba wako. Juzi tena huyu msichana wa kazi akaukuta ule mkoba chini ya uvungu wa kitanda. Nikakuuliza huu mkoba ni wa nini ukajidai kuniambia ulipewa na babu yako…”
Hapo nikanyamaza. Kule kunyamaza kwangu kukampa nafasi ya kuendelea kunichamba.
“Mkoba una hirizi, una mkono wa mtoto mchanga umekauka, kama si uchawi ni kitu gani? Basi huyo babu yako pia alikuwa mchawi ndiyo maana alikupa ule mkoba. Usinidanganye mume wangu, wewe ni mchawi. Na sasa mtoto wako anatakiwa na mimi sitakuwa tayari achukuliwe. Nitakuumbua!”
Maneno ya mke wangu yalikuwa yakiniingia akilini na kunichoma moyo. Nilibaki kunyamaza huku nikichezea rimoti ya TV.
Sikujua kama aliona ule mkono wa mtoto mchanga uliokuwa kwenye mkoba wangu. Inaelekea aliuchunguza sana.
Alikuwa na ushahidi wa kutosha wa kunitia katika hatia, ilinipasa ninyamaze tu. Kwanza ule mkono wa mtoto mchanga kama utaonekana na polisi ninaweza kushitakiwa na kupoteza uwaziri wangu pamoja na ubunge. Isitoshe mke wangu alikuwa ameyakariri vyema maelezo ya wale wachawi yanayoashiria kuwa mimi pia ni mchawi.
“Sasa mimi naondoka na mwanangu. Siwezi kuendelea kuishi na wewe. Mwanangu atachukuliwa, mtoto mwenyewe ameshalegea, sijui wameshamchukua kivuli?”
Niliona kunyamaza zaidi kutampa nguvu mke wangu na kuendelea kuamini moja kwa moja kuwa mimi ni mchawi. Nikamwambia.
“Unanituhumu bure tu, mimi si mchawi na wala sijapanga kumtoa mtoto wangu kwa wachawi. Usidhani mimi sina akili nizae mtoto kisha niwape wachawi wamle!”
“Uliwaahidi, hivi sasa umewageuka wenzako ndiyo maana wanakufuata nyumbani,” mke wangu alisisitiza.
Nikanyamaza tena kwa sababu alichosema kilikuwa ni cha ukweli na ukweli ukidhihiri, uongo hujitenga.
“Leo atachukuliwa mtoto na kesho nitachukuliwa mimi, bora nijiepushe mapema. Naenda kwetu.”
Akilini mwangu nilikuwa ninawaza jinsi ya kuepukana na aibu ile.
Je, kilifuatia nini? Usikose mwendelezo wake katika Gazeti la Ijumaa siku ya Ijumaa.
Post a Comment

Our Team

Video of the Day

Contact us

Name

Email *

Message *