Monday, 29 February 2016

Kinara Uporaji Benki Mbagala Atiwa Mbaroni

INNOCENT-THE BLOGGER-BOY

Siku nne baada ya majambazi 12 kuvamia Benki ya Access tawi la Mbagala, jijini Dar es Salaam na kuiba Sh. milioni 20 na kusababisha vifo vya watu saba, mtu anayedaiwa kuwa kinara wa uhalifu huo ametiwa mbaroni baada ya kutajwa na washirika wake, akiwamo aliyekamatwa  akiwa anafunga ndoa.

Taarifa za uhakika  zinaeleza kuwa, kinara wa ujambazi huo alikamatiwa Sinza Mori, wilaya ya Kinondoni jana, saa 11:00 jioni.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, kikosi kinachoshirikisha askari wa majeshi mbalimbali ikiwamo, polisi na la wananchi wa Tanzania, kilinasa watu wanne kwenye sherehe ya harusi baada ya kufuatilia mawasiliano yao ya simu.

“Unajua sasa hivi hili suala linahusisha jeshi ambao wamefuatilia kwenye mtandao na kunasa simu za watu wanne ambao wamekamatwa huko Mbagala, akiwamo bwana harusi na watu wengine wanne,” kilisema chanzo cha habari hii.

Taarifa hizo zinasema baada ya watu hao kukamatwa wakiwa wanafunga ndoa msikitini, walisaidia kutoa taarifa ambazo hatimaye zilifanikisha kukamatwa kwa mtu huyo anayedaiwa kuwa ni kinara wa ujambazi huo.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro, alipoulizwa kuhusu tarifa hizo alisema bado hajazipata na kwamba yawezekana wasaidizi wake wamemkamata lakini bado hawajamfikishia taarifa.

Kinara huyo amekamatwa ikiwa imepita siku moja baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, kutangaza uwezekano wa kutumia Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kushirikiana na polisi kuwasaka wahalifu wote waliojificha kwenye misitu ya Bagamoyo na Pwani, ambako inadaiwa walikimbilia baada ya tukio la Mbagala.

Pia waziri huyo alisema katika operesheni hiyo, watakuwa wakiwasimamisha mara kwa mara watumia pikipiki kwa sababu vyombo hivyo vimekuwa vikitumiwa na majambazi katika kufanikisha matukio yao.
Post a Comment

Our Team

Video of the Day

Contact us

Name

Email *

Message *