Monday, 22 February 2016

Jecha: Tunamtambua Maalim Seif mgombea

INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha

LICHA ya Chama cha Wananchi (CUF) na vyama vingine sita vya siasa kuandika barua ya kueleza kutoshiriki Uchaguzi Mkuu wa marudio uliopangwa kufanyika Machi 20, mwaka huu, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha amesema ofisi yake bado inawatambua wagombea wa vyama hivyo.
“Mgombea Urais wa CUF na wagombea wake wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani, na vyama vingine sita waliandika barua kwa ZEC wakisema hawatashiriki uchaguzi huo. Kwa bahati mbaya, wagombea wote na vyama vyao vya siasa vinavyodai kususia, wameshindwa kufuata taratibu.
“Inaelezwa wazi katika Kifungu cha 31 na 37A na Sura ya 46 na 50 ya Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, kuhusu taratibu za uteuzi wa wagombea na jinsi gani wagombea wanaweza kujitoa katika uchaguzi. Hakuna hata mgombea mmoja aliyefuata sheria hiyo,” alisema Jecha katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana.
Jecha alisema kulingana na kanuni, ni jukumu la chama cha siasa kuandika kwa ZEC kuhusu kuondoa udhamini wake kwa mgombea. Alisema hata CUF ambayo mgombea wake ni Maalim Seif Shariff Hamad, imeshindwa kufuata kanuni hizo.
“Ni muhimu sana kuelewa na kufuata sheria za uchaguzi. Tumekuwa tukiwasiliana na vyama vyote 14 vya siasa, sambamba na kusambaza vifaa vya uchaguzi kwa wilaya zote kumi na moja kabla ya kuvitawanya baadaye kwenye vituo 1,580 vya kupigia kura,” alisema Jecha.
Alisema wagombea wote 14 wa urais, watu wanaowania Uwakilishi kutoka katika majimbo 54 na wagombea 111 katika ngazi ya Udiwani, bado wanaendelea kutambulika kama wagombea halali kwa uchaguzi wa mwezi ujao.
Jecha amekiri kupokea barua kutoka CUF na vyama vingine sita wakisema hawatashiriki uchaguzi huo, wakati vyama vingine vinane kikiwamo CCM, ACT, ADC CCK AFP, SAU, TLP na ADA-TADEA vimethibitisha kushiriki.
“Tunakamilisha taratibu ili kuwapatia wagombea wote wa urais ulinzi kwa saa 24 hadi wakati matokeo ya uchaguzi yatakapokuwa yametangazwa,” alisema Jecha na kuongeza kuwa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura litawekwa katika sehemu mbalimbali ili wapiga kura waone vituo vyao vya kupigia kura.
Alisema kuwa maandalizi kwa ajili ya marudio ya uchaguzi huo yanaendelea vizuri na tayari uteuzi na kuajiri maofisa wa uchaguzi na wafanyakazi wengine umefanyika na kufuatiwa na mafunzo kuhusu jinsi gani ya kusimamia vizuri uchaguzi.
Alisema mafunzo kwa ajili ya wasimamizi wa uchaguzi (ngazi ya majimbo) yanatarajiwa kuanza leo hadi Februari 28, wakati mafunzo kwa maofisa wa vituo vya kupigia kura yataanza Machi 11 hadi 13, mwaka huu.
Mafunzo kwa ajili ya mawakala wa vyama vya siasa na maofisa wa kusimamia usalama yatafanyika Machi 14 na 15, mwaka huu, kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo wa ZEC.
Mwenyekiti huyo wa ZEC alisema maandalizi ya awali ya kuchapisha karatasi za kura yamekamilika, na mchapaji ambaye hakutaka kumtaja anaendelea na kazi ya kuchapa karatasi hizo ambazo zinatarajiwa kuletwa Zanzibar mapema mwezi ujao.
“Tunawaomba wananchi wajiandae kwa uchaguzi wa marudio na wagombea wote kutoka vyama tofauti vya siasa kufuata kanuni na sheria za uchaguzi,” alisema Jecha.
Uchaguzi huo wa marudio wa Machi 20, mwaka huu utafanyika baada ya ule wa Oktoba 25, mwaka jana, kufutwa kutokana na kasoro mbalimbali zilizoufanya usiwe huru na wa haki. Juhudi za kuwapata wasemaji wa CUF jana hadi tunaenda mitamboni hazikufanikiwa.
Post a Comment

Our Team

Video of the Day

Contact us

Name

Email *

Message *