Wednesday, 4 November 2015

RC Dar aonya wanaoamsha hisia za uvunjifu wa amani

INNOCENT-THE BLOGGER-BOY


VIONGOZI wa vyama vya siasa wametakiwa kuheshimu Katiba ya nchi kwa kuacha kuendeleza mgogoro na kuamsha viashiria vya uvunjifu wa amani ya nchi kwa madai ya kutokukubaliana na matokeo ya Urais yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). 

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki aliyasema hayo jana wakati akizungumza kwenye mkutano wa Kamati ya Amani ya viongozi wa dini wa madhehebu mbalimbali na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Dar es Salaam uliofanyika jana Dar es Salaam. 

Alisema kwa mujibu wa Katiba ya nchi NEC pekee ndiyo yenye mamlaka ya kutangaza matokeo na ikishafanya hivyo hakuna mahali pa kwenda kupinga. Alisema wanasiasa hao kwa kusambaza taarifa za kufanya maandamano ya kupinga matokeo hayo ni uchochezi na kukiuka sheria za nchi ambapo kunaweza kusababisha uvunjifu wa amani. 

“Wapo watu ambao hawataki kuheshimu hilo, wanasambaza meseji za uchochezi ambazo zinaweza kuvuruga amani yetu …” alisema Sadiki. Aliwaomba viongozi hao wa dini kuendelea kuhubiri amani kwani kamati hiyo imefanya kazi kubwa katika kuhakikisha nchi inapita salama katika uchaguzi licha ya kuwepo kwa matukio madogo ya uvunjivu wa amani. 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Salum alisema katika kipindi cha kuanzia kampeni, upigaji kura na baada ya uchaguzi, mambo yameenda vizuri kwa kuwa amani imetawala. 

Alisema kutokana na amani kutawala hata baadhi ya mataifa mengine ambayo yalikuwa yakitamani kuona Tanzania ikiingia katika machafuko yamepata mshangao kuona bado amani inaendelea kuwepo. 

Hata hivyo, alitaka wagombea ambao hawakuridhika na matokeo yaliyotolewa wafuate taratibu badala ya kuwashawishi na kuwatumia wananchi kuingia barabarani na kufanya vurugu na maandamano. “Walioshindwa wasiwatumie Watanzania kuingia barabarani kufanya vurugu, tuheshimu damu za Watanzania,” alisema Sheikh Alhad.
Post a Comment

Our Team

Video of the Day

Contact us

Name

Email *

Message *