Saturday, 7 November 2015

Polisi Yawahoji Tena Watumishi 38 LHRC

INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limekitaka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kuwa watulivu na kusubiri jeshi hilo likamilishe upelelezi wake juu ya tuhuma za watumishi wake kukusanya na kusambaza taarifa zisizo sahihi wakati wa uchaguzi mkuu uliofanyika hivi karibuni. 

Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na Kamishna wa Polisi wa Kanda Maalumu Suleiman Kova wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya jana kuwahoji kwa mara ya pili viongozi na wafanyakazi 38 wa kituo hicho wanaotuhumiwa kukusanya na kusambaza taarifa zisizo sahihi kinyume na sheria ya udhibiti wa makosa ya mtandao. 

“Lazima watulie na kuliachia jeshi kuendelea na upelelezi wake na ukikamilika upelelezi basi jalada litapelekwa kwa mwanasheria wa serikali na mpaka kufikia Jumatatu ijayo tutajua hatima ya watuhumiwa pamoja na vielelezo vyao,” alisema Kova. 

Aliongeza kuwa, katika mahojiano ya awali ilibainika kituo hicho kilichopo Mbezi Beach kilipewa kazi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwa waangalizi wa ndani wa uchaguzi na kupewa masharti ya namna ya kutekeleza kazi hiyo ikiwa ni pamoja na kutokutoa maoni na taarifa yoyote kwa vyombo vya habari au umma juu ya mchakato wa uchaguzi wakati wa upigaji kura ukiendelea.

“Kwa sababu hizo sasa tumeendelea kuwahoji ili watoe ufafanuzi kutokana na yale yaliyogundulika na jeshi letu kwamba ni kinyume cha sheria za mtandao pamoja na sheria ya uchaguzi kanuni na maelekezo ya NEC kwa waangalizi wa uchaguzi wa ndani na nje,” alisema Kova. 

Aidha, alisema jeshi hilo kupitia Kitengo cha Sayansi ya Uchunguzi wa Makosa ya Jinai kimegundua kuna makosa ya jinai yaliyotendeka kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii nchini sambamba na hilo pia zipo tuhuma kwamba kituo hicho kilikiuka sheria ya uchaguzi pamoja na maelekezo ya NEC ya mwaka 2015 kuhusu maelekezo na masharti waliyopewa waangalizi wa ndani na nje ambavyo vinazungumzia kuheshimu na kutii sheria za Tanzania. 

Hata hivyo, Mkurugenzi wa LHRC, Dk Hellen Kijo-Bisimba amelitaka jeshi hilo kuharakisha upelelezi wake kwani vifaa vilivyochukuliwa vina kazi muhimu za taasisi yao na kwamba wanapaswa kutoa taarifa kwa yale waliyoyafanya katika kipindi chote cha uchaguzi.
Post a Comment

Our Team

Video of the Day

Contact us

Name

Email *

Message *