Monday, 16 November 2015

Lowassa Ataja Sababu 4 Kumpinga Magufuli.....Zifahamu Hapa

INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
Aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) chini ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa (wa pili kulia), akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana juu ya hali ya kisiasa nchini. Wengine ni Kaimu Mwenyekiti wa Cuf, Twaha Taslima (wa kwanza kushoto), Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Prof. Abdallah Safari (wa pili kushoto) na Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia (wa kwanza kulia). PICHA: MPOKI BUKUKU
Aliyekuwa mgombea urais kupitia  Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, ameeleza sababu za kutokubaliana na ushindi uliomuweka madarakani mpinzani wake kupitia CCM, Dk. John Magufuli katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Aidha, amewataka Watanzania kutoyakubali matokeo hayo na kuyapinga kwa nguvu zao zote bila ya kuandamana na kufanya fujo na kwamba umoja huo hautashirikiana na serikali ya Dk. Magufuli kwa madai haikuingia madarakani kihalali. 
 
Lowassa alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa jijini Dar es Salaam jana juu ya hali ya kisiasa nchini na mustakabali wa Zanzibar baada ya kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa visiwa hivyo.
 
ATAJA SABABU ZA KUPINGA
Lowassa alisema yeye na wenzake ndani ya Ukawa hawaukubali na ushindi alioupata Dk. Magufuli kwani wana ushahidi wa kutosha juu ya namna Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake kilivyopora ushindi wake (Lowassa) kwa kuyakachakua matokeo.
 
Hata hivyo, Lowassa hakuwa tayari kuuweka wazi ushahidi, akisema atafanya hivyo wakati muafaka ukifikaa ambao pia hakuutaja. 
 
Alitaja sababu nyingine za kutokukubali na ushindi wa Dk. Magufuli kuwa ni, matumizi makubwa ya vyombo vya dola wakati wa uchaguzi. 
 
Alisema wakati wa uchaguzi huo serikali ilitumia nguvu kubwa na vitisho vya askari wenye silaha za kivita ikiwamo kutumia magari yenye maji ya kuwasha yaliyonunuliwa kwa mabilioni ya fedha, ambayo yalikuwa yanarandaranda mitaani, ili matokeo aliyodai ya wizi huo wa kura yakubalike.
 
Sababu nyingine aliyoitoa Lowassa ni hatua ya serikali kupinga maandamano ya Ukawa na kuvitisha vyombo vya habari kufanya kazi zake kwa uhuru.
 
Nyingine alisema ni hatua ya serikali kupiga marufuku mikutano ya kisiasa iliyopangwa  kufanywa na viongozi wa Ukawa na kuwanyima viongozi hao fursa ya kuwashukuru wananchi kwa kuwapigia kura baada ya uchaguzi.
 
 “Wanatumia gharama zote hizo huku bei ya vitu mbalimbali hasa vyakula inapanda kwa kasi kubwa, kama CCM inadai imeshinda kwa nini wana hofu kubwa mpaka kuhujumu uhuru wa vyombo vya habari, kupiga marufuku mikutano ya kisiasa na kunyima viongozi wa Ukawa hata fursa ya kuwashukuru wananchi kwa kutuunga mkono katika safari yetu ya kuleta mabadiliko, hii ni aibu kwa taifa letu,” alisema Lowassa na kuongeza:
 
“Tuna ushahidi wa kutosha jinsi matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano yalivyochakachuliwa na kiasi cha kura zilizoibwa, wakati muafaka tutaweka bayana ushahidi huo ili Watanzania wajue kwa nini Ukawa inasema kwa dhati kwamba haitambui matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na kwa nini haitashirikiana na serikali ya sasa ambayo ni batili kisheria.”
 
Lowassa alisema endapo Katiba ingekuwa inaruhusu matokeo ya urais kupingwa mahakamani wangefanya hivyo, lakini kwa kuwa hairuhusu wataendelea kutoitambua serikali hiyo, huku akiwataka wananchi kukataa matokeo hayo katika hali ya utulivu wakati Ukawa ikiendelea na harakati nyingine za kisiasa katika nyanja mbalimbali ili kutekeleza azma yao ya kuleta mabadiliko ya kweli nchini.
 
ZANZIBAR
Aidha, Lowassa alisema Ukawa unamuunga mkono mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi(Cuf), Maalim Self Sharif Hamad, kama mshindi wa uchaguzi mkuu visiwani humo na kuitaka Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) imtangaze mara moja.
 
Alisema kinyume na Tanzania Bara ambako uchaguzi uligubikwa na mizengwe, uchaguzi wa Zanzibar ulikuwa wazi na wa amani, huku vyama vyote vya siasa na hata waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa walisema uchaguzi huo ulifanyika kwa amani, lakini wanashangaa Zec kufuta uchaguzi huo.
 
Alisema uamuzi huo wa Zec unalaaniwa vikali na Ukawa na kwamba uamuzi wa kutaka uchaguzi huo urudiwe  hawakubaliani nao kwa kile alichosema  hizo ni mbinu mpya ambazo zimepangwa kuhujumu uchaguzi huo na una lengo  la kuhatarisha  amani na utulivu visiwani humo. 
 
“Wakuu wa Ukawa walikataa dhana kuwa uchaguzi uleule unaodaiwa kufutwa kwa kuwa ulikuwa na mizengwe, ulizaa matokeo halali ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya urais wa Jamhuri, lakini ni batili kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Rais wa Zanzibar, dhana hii haina mantiki yeyote bali ni ubabe wa kisiasa,” alisema Lowassa na kuongeza:
 
“Haiwezekani chungu kimoja kikapika halali na haramu kwa pamoja. Kigezo cha Zec kuwa uchaguzi wa Zanzibar ulikuwa batili, basi matokeo yake yote ikiwa ni pamoja na yale ya urais wa Jamhuri pia ni batili. Hii ina maana kuwa hata ushindi unaodaiwa wa Dk. Magufuli, mbali ya kuwa ni matokeo haramu ya wizi kwa kura za Tanzania Bara, pia ni batili kisheria kwani hana ridhaa ya watu wa pande zote mbili za Muungano.”
 
KATIBA MPYA
Lowassa alisema bado wataendelea kupigania kuandikwa kwa Katiba mpya ambayo watahakikisha inazingatia maoni na matakwa ya Watanzania.
 
Alisema pasipo Katiba hiyo, matatizo mengi yanayojitokeza hivi sasa hayatapatiwa ufumbuzi  ikiwamo kuwa na tume huru ya uchaguzi na serikali inayowajibika, huku akisisitiza kuwa katika mazingira ya sasa na chini ya Katiba inayotumika sasa, Tanzania haitakuwa na demokrasia na itaendelea kuwa nchi inayotawaliwa kwa mizengwe na udikiteta .
 
AELEZA HATMA YAKE 
Lowassa alisema hatarudi nyuma wala kustaafu siasa, bali ataendelea kuimarika katika nyanja hiyo kwa kuwa mstari wa mbele kupigania Ukawa na mabadiliko.
 
MBATIA
Kwa upande wake, Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia, alisema vurugu zinazoendelea hivi sasa na mauaji ya Watanzania  katika matukio tofauti na matumizi ya mabavu, itafika mahali Watanzania watakosa uvumilifu na endapo machafuko yakitokea Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete  pamoja na Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva, wote watafikishwa katika mahakama za kimataifa.
 
Mbatia  alidai Kikwete atawajibika pamoja na mambo mengine kwa kutumia nguvu kubwa kununua vifaa vya kivita vyenye thamani ya Sh. bilioni 409 katika uchaguzi wa mwaka huu, huku akimtaja Jaji Lubuva kwamba atawajibika kwa kukiuka sheria za uchaguzi kwa kuibeba CCM na Mkapa atawajibika kwa kusababisha mauaji katika uchaguzi Mkuu 2001, Zanzibar.
 
Akizungumzia kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo, aliyeuawa juzi kwa kukatwa mapanga na watu wasiojulikana, Mbatia alihusisha kifo chake na mauaji mengine ambayo yamekuwa yakihusishwa na chuki za kisiasa.
 
Lowassa aliungana na Mbatia kulaani mauaji hayo na kulitaka Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa haraka ili kubaini waliohusika na kuwachukulia hatua.
 
MALALAMIKO VITI MAALUM
Akizungumzia malalamiko kutoka maeneo mbalimbali nchini kuhusu mgawanyo wa viti maalum kwenye nafasi ya ubunge ndani ya Chadema, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Prof. Abdallah Safari, alisema Chadema imepokea malalamiko mengi kuhusiana na mgawanyo wa wabunge wa vitihivyo na kwamba kinayafanyia kazi na yale ya msingi yatafanyiwa uamuzi na yasiyo ya msingi yataachwa.
 
Naye Kaimu Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (Cuf), Twaha Taslima, alisema masuala ya wabunge wa viti maalum yanazungumzwa ndani ya chama na si katika vyombo vya habari.
 
Katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu, Nec ilimtangaza Dk. Magufuli wa CCM kuwa mshindi wa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano kwa kupata  asilimia 58.46 ya kura halali zilizopigwa, huku Lowassa akipata asilimia 39.97.
 
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment

Our Team

Video of the Day

Contact us

Name

Email *

Message *